Tafuta katika Blogu Hii

Jumatatu, 19 Januari 2015

Lema, Nassari Wadai watamtoa Muhongo Bungeni kwa Mabavu

By. Bongoplanet Media Group
Mbunge wa Arusha mjini (Chadema) Godbless Lema amesema atamtoa kwa mabavu bungeni Waziri wa nishati na madini,Profesa Sospetre Muhongo katika kikao kijacho cha Bunge endapo atakuwa hajaondolewa kwenye nafasi hiyo.

Mkakati huo wa Lema umeungwa mkono na Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari ambaye pia amepanga kumtoa bungeni kwa nguvu, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge.

“Keshokutwa nakwenda bungeni kufanya kazi moja tu, nikimkuta Muhongo bungeni ndipo nitafukuzwa ubunge moja kwa moja,” alisema Lema huku akishangiliwa wananchi na kuongeza; “Nikimkuta Muhongo bungeni na Chenge bado ni viongozi mimi nitakwenda kumshika Muhongo nimtoe bungeni kwa sababu Katiba inaruhusu kila raia kukemea uovu.”

Profesa Muhongo na Chenge ni miongoni mwa viongozi ambao Bunge liliazimia wawajibishwe na mamlaka zao kutokana na kashfa ya uchotwaji mamilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Hata hivyo, wakati Rais Jakaya Kikwete akilihutubia Taifa, Desemba 22 mwaka jana kupitia wazee wa Dar es Salaam, alitangaza kumweka kiporo Profesa Muhongo kwa siku mbili au tatu, ahadi ambayo haijatekelezwa.

Tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema anayehusishwa na sakata hilo alishatangaza kujiuzulu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka akifutwa kazi.

Hakuna maoni: